Arusha
Home » » TEMBO WAVAMIA MAKAZI, WAUA, KUJERUHI

TEMBO WAVAMIA MAKAZI, WAUA, KUJERUHI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mkuu wa Wilaya ya Longido, James Ole Millya
 
Kundi la tembo limevamia makazi ya wananchi wa Kata ya Tingatinga, Wilaya ya Longido, mkoani Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na mwingine kujeruhiwa.
Katika hekaheka ya kukabiliana na tukio hilo, tembo mmoja ameuawa kwa ushirikiano wa wananchi na askari wa wanyamapori kutoka Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kaskazini.

Wananchi wa kata hiyo, waliliambia NIPASHE kuwa aliyeuawa na tembo hao ni mtoto  wa miaka tisa aliyetajwa kwa jina la Fred Joseph, huku Paulo Lukari, akijeruhiwa na kulazwa hospitali. 

Wakizungumza baada ya Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Kaskazini kufika na  kushirikiana nao kumuua tembo aliyesababisha madhara hayo, wananchi hao  wamelalamikia watendaji wa sekta ya wanyamapori kwa kuendelea kukaa mijini na  kusubiri kupewa taarifa wakati wananchi vijijini wakiendelea kuuawa.

Diwani wa Kata ya Tingatinga, Sabore Olemoloimet, ameiomba serikali kuhakikisha  watendaji wanaoshughulikia migogoro ya wananchi na wanyamapori kuhamia maeneo  husika ili wawadhibiti wanyama kabla hawajaleta madhara.

“Kuna haja ya watendaji wa sekta hii kuwa karibu na wananchi, hasa kwenye maeneo hayo, ambayo yamekuwa yakilalamikiwa kila siku na wananchi, kwani pamoja na umuhimu wa wanyamapori tatizo hili linawaongezea wananchi umaskini,” alisema Sabore Olemoloimet, ambaye ni Diwani Kata ya Tingatinga.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, James Ole Millya, alithibitisha kuwapo kwa udhaifu mkubwa kwa watendaji wanaoshughulikia wanyamapori na kwamba, licha ya kutoa  maelekezo mara kadhaa bado hayafanyiwi kazi.

“Nimeshamwandikia mkurugenzi barua, lakini naona bado hajachukua hatua. Itabidi nichukue hatua zaidi kwa ngazi za juu,” alisema Millya. 
Baada ya tembo huyo kuuawa, makundi ya wananchi wa eneo hilo yalifika na kuanza  kugawana kitoweo, huku wakimshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuondokana na tatizo hilo na pia kupata kitoweo.

Baadhi walitaka wapewe kipaumbele kwa kupewa nyama nyingi kwa madai kuwa wameathirika zaidi na wanyama hao. 

Vilio vya wananchi juu ya madhara yanayosababishwa na wanyamapori, wakiwamo  tembo vimekuwa vikisikika katika kona mbalimbali nchini jambo linaloonyesha kuwa  bado tatizo hilo halijapata ufumbuzi wa kudumu.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa