Arusha
Home » » SEKTA BINAFSI SASA YASHIKA UCHUMI EAC

SEKTA BINAFSI SASA YASHIKA UCHUMI EAC

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Meneja Biashara wa Kampuni ya Kuhudumia Makontena Bandarini, Predi Assenga (kushoto) na Meneja wa Kitengo cha Makontena, Donald Talawa wakiangalia meli ya kubeba mitambo mizito Zhen Hua wakati ikitia nanga Dar es Salaam jana
Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Richard Sezibera amesema nchi wanachama wa jumuiya hiyo zinajengwa na sekta binafsi ambayo ndiyo injini ya uchumi wake.
Akizungumza baada ya kufungua duka la Nakumatt jijini Arusha, Dk Sezibera alisema: “Tunaamini kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wa Afrika Mashariki na sisi tutahakikisha wananchi wa nchi wanachama wanafaidika na ukuaji wa uchumi wa jumuiya kupitia fursa za kibiashara zinazopatikana EAC.”
Kampuni ya Nakumatt iliyonunua mali zote zilizokuwa chini ya maduka ya Shoprite nchini, imewekeza zaidi ya Dola za Marekani 2 milioni (Sh3.3 bilioni) mkoani Arusha na kuwawezesha vijana 50 kupata ajira za kudumu.
Dk Sezibera aliupongeza uongozi wa kampuni hiyo kwa kufungua duka hilo. Ufunguzi huo unafikisha idadi ya maduka ya Nakumatt (Nakumatt Supermarkets) katika nchi zote za EAC kufikia 50, huku Tanzania ikiwa na manne.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Nakumatt, Atul Shah alisema kuwa ndoto yake ya muda mrefu ni kuwekeza sehemu kubwa ya Afrika na kuwafaidisha maelfu ya wakulima na wenye viwanda.
Alisema sera ya kampuni yake ni kuendeleza wakulima na wazalishaji wa nchi za Afrika, ambako kampuni hiyo inafanya nao biashara.
Meya wa Jiji la Arusha, Mstahiki Gaudence Lyimo alisema kuwa kufunguliwa kwa duka hilo kutaongeza hadhi ya jiji hilo na kuomba wawekezaji wengine kujitokeza kuwekeza.
“Tumefurahishwa na uwekezaji huu…biashara hii italeta huduma zenye unafuu kwa watu wa kada za juu, kati na chini na utatuongezea mapato,” alisema Lyimo.
Nakumatt ambayo tayari ina maduka Mlimani City na Kamata jijini Dar es Salaam na Moshi mkoani Kilimanjaro na Arusha, imeajiri jumla ya watu 7,500 katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa