Arusha
Home » » LOWASA:MAPATO YA GESI YASAIDIE ELIMU

LOWASA:MAPATO YA GESI YASAIDIE ELIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Lowassa: Mapato ya gesi yasaidie elimuWAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amesema kuwa elimu hapa nchini iko hoi, kwamba unahitajika ushirikiano wa pamoja baina ya wadau pamoja na kutumia mapato ya gesi kuinusuru.
Lowassa ameishauri serikali kuangalia uwezekano wa kutumia mbinu zilizotumiwa na nchi ya Marekani kuboresha elimu yao kwa kuwachukua wataalam waliobobea kwenye sekta hiyo na kuwafungia mahali kwa miezi sita kisha wakatoke na majibu ya kumaliza tatizo hilo.
Alitoa rai hiyo jana wakati akifungua mkutano wa 25 wa Dayosisi ya Kaskazini Kati ambapo pamoja na mambo mengine, utamchagua askofu wa dayosisi hiyo kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Askofu Thomas Laizer aliyefariki mwaka jana.
Lowassa alisema kuwa elimu imeendelea kuwa hoi licha ya kuundiwa tume mbalimbali ambazo hazileti taarifa hadharani jambo alilodai linasababisha kushindwa kuelewa anayekosea ni nani kati ya tume na serikali ambayo haitekelezi mapendekezo ya tume hizo.
“Angalieni wanazungumza habari ya kufaulu kwa kupata daraja A ambalo halifanani na mahali popote duniani, haiwezekani lazima kuna tatizo mahali, lazima tukubali ni wajibu wetu,” alisema.
Alisema kuwa kuna ulazima wa kugawana majukumu na kila mmoja kutimiza wajibu wake ikiwemo serikali, wazazi, wanafunzi na kanisa ambapo kila mmoja abebe mzigo wake kuhakikisha elimu inaboreka.
“Mwenyezi Mungu ametubariki tumepata gesi, wanasema msipoangalia gesi inaweza kugeuka kuwa laana, mimi nafikiri mahali pa kuelekeza fedha za gesi ni kwenye elimu bora.
“Elimu itakayojibu mahitaji ya sasa badala ya kuendelea kuwasumbua wazazi huko vijijini wenye hali mbaya, tunaweza kutumia fedha za serikali na kanisa kuwaokoa hawa wazazi wasio na uwezo,” alisema.
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, aliongeza elimu itakayotolewa ilenge kutoa ajira kwa wahitimu kwani kwa sasa kuna tatizo kubwa la ajira nchini.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa