Arusha
Home » » CWP WAKERWA UTEKAJI WASICHANA NIGERIA

CWP WAKERWA UTEKAJI WASICHANA NIGERIA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa CWP, Rebeca KidagaWABUNGE wanawake wa mabunge ya Jumuiya ya Madola, (CWP), wameitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kushirikiana na Serikali ya Nigeria, kuhakikisha watoto wa kike 200 wanaoshikiliwa na kundi la kigaidi la Boko Haram wanaachiwa.
CWP ukanda wa Afrika wamepanga kwenda Nigeria kwa ajili ya kuzungumza na wanawake na Rais Goodluck Jonathan, kujua kwanini hadi sasa watoto hao hawajaachiwa.
Kauli hiyo ilitolewa kwa nyakati tofauti jana jijini hapa na Mwenyekiti wa CWP, Rebeca Kidaga na Makamu Mwenyekiti wa CWP, Ukanda wa Afrika, Beatrice Shelukindo, walipokuwa wakitoa msimamo wa vyombo hivyo katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA), Kanda ya Afrika.
Kidaga ambaye pia ni Spika wa Bunge la Uganda, alisema wameumizwa na tukio hilo huku wakitaka Serikali ya Nigeria na jumuiya za kimataifa kuhakikisha matukio ya kigaidi ya Boko Haram yanakomeshwa.
Naye Shelukindo, alisema watakwenda Nigeria kabla ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika Aprili mwakani.
Awali akiwasilisha mada kwenye mkutano huo juu ya changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa malengo ya milenia, kwenye elimu ya msingi kwa watoto wa kike, Shelukindo, alisema Tanzania imefanikiwa kwani kwenye baadhi ya maeneo idadi ya watoto wa kike wanaojiunga na shule imekuwa sawa huku baadhi ya maeneo ikiwa kubwa zaidi.
Hata hivyo, alisema kuwa suala la uhamasishaji wanawake kujiunga na masomo ya sayansi bado linakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na hulka na mazoea mabaya yaliyojengeka kwenye jamii kuwa wanawake hawawezi uhandisi sanjari na wao wenyewe kutojiamini.
“Kwa mfano ni vigumu kwa mwanamke aliyeolewa na  aliyeajiriwa na kampuni ya simu kutoka nyumbani kwake usiku kwenda kushughulikia tatizo lililojitokeza kwenye mitambo, mwaka 2009 kuna utafiti ulionyesha kwamba wanawake wanasayansi wanakwazwa na waume zao kutokana na utaratibu uliopo kuwa wanawake husikiliza uamuzi wa waume zao na kuwaheshimu, hivyo wamekuwa kikwazo,” alisema Shelukindo.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa