Arusha
Home » » MLIPUKO WATOKEA KATIKA MKUTANO WA CHADEMA, BOMU LAJERUHI NA KUUA JIJINI ARUSHA

MLIPUKO WATOKEA KATIKA MKUTANO WA CHADEMA, BOMU LAJERUHI NA KUUA JIJINI ARUSHA




 


Majeruhi. Mungu urehemu tz
ARUSHA.
MKUTANO wa Chadema wa kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani mjini Arusha, jana ulivunjika baada ya bomu kulipuka na kuua watu wanne na wengine kujeruhiwa.
Bomu hilo lililipuka jana saa 11:50 dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Soweto mjini Arusha na kuhudhur iwa na mamia ya wananchi.
Hilo ni tukio la pili la bomu kulipuka katika mkusanyiko wa watu, Mei 5 mwaka huu bomu lililipuka katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit mjini Arusha na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru Frida Mokiti alisema katika hospitali yake kuna maiti moja ya mtoto na majeruhi 11.
Habari zingine zilisema katika hospitali ya Misheni ya Selian kuna maiti za watu wawili, waliokufa kutokana na shambulio hilo na majeruhi ambao idadi yao haijafahamika.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema katika tukio hilo watu wawili wamepoteza maisha, mwanamke na mwanamume na kwamba idadi ya majeruhi bado haijafahamika kwa kuwa wametawanywa katika hospitali mbalimbali mkoani humo.
Watu walioshuhudia tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa bomu hilo lililipuka karibu na jukwaa walilokuwa wamekaa viongozi wa Chadema, wakati Mbowe na Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema wakiwa katika hatua za kumaliza kuhutubia.
Taarifa zilidai kuwa kuna mtu alionekana akirusha kitu kinachodaiwa bomu kwenye eneo la jukwaa karibu na gari la matangazo la chama hicho, lakini alipokuwa akifuatiliwa baada ya kutokea mlipuko huo, polisi nao walikuwa wameanza kudhibiti watu kwa kulipua mabomu ya kutoa machozi na kupiga risasi za moto hali iliyozidisha taharuki.
Baada ya tukio hilo watu waliokuwa katika mkutano huo walitawanyika wakikimbia kuokoa maisha yao huku wakimwacha Mbowe na Lema na viongozi wengine wakiwa bado wako jukwaani.
Hali hiyo ilifanya barabara zote za mji wa Arusha kujaa watu waliokuwa wakikimbia ovyo.
Hali hiyo ya watu kukimbia ovyo kuliwafanya askari polisi wengi kuingia mitaani kudhibiti watu na hivyo nao kulazimika kutumia mabomu ya machozi hali ambayo ilizidisha taharuki.
Baadhi ya watu waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na wengine katika Hospitali ya Seliani na wafuasi wa Chadema na watu wengine waliokuwa katika eneo hilo. CHANZO MWANANCHI.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa